Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imetoa wito wa kufanyika maombi ya kitaifa yakitanguliwa na mfungo wa siku tatu kuanzia kesho, kuiombea nchi kufuatia tukio la vurugu lililotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, lililosababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu.

Akizungumza leo Dodoma, Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, amesema matukio hayo yameacha majeraha ya kisaikolojia na kuchochea hisia za kidini, hivyo kunahitajika hatua za haraka kuimarisha umoja wa kitaifa. Amehimiza maombi hayo yashirikishe waumini wa madhehebu zote na kufanyika kwa mfumo mmoja na Kwa siku moja kitaifa.
JMAT pia imelaani vikali kauli za baadhi ya viongozi wa dini zinazochochea mgawanyiko kati ya Waislamu na Wakristo, ikisisitiza kuwa hakuna vita vya kidini nchini. Aidha, imeshauri kufanyika maridhiano ya kisiasa yakihusisha Rais, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini wenye misimamo ya haki.

Katika hatua nyingine, JMAT imetoa wito kwa wananchi hasa vijana kuepuka kushiriki maandamano au vurugu zinazopangwa kufanyika Desemba 9, 2025, ikiitaja siku hiyo kuwa ni ya heshima ya Taifa.

Jumuiya hiyo pia imempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua ya kulifungua Kanisa la Ufufuo na Uzima, ikisema ni ishara ya kuheshimu uhuru wa dini. Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa JMAT Askofu Dkt. Israel Maasa amependekeza kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii, ikitajwa kuwa chanzo kikuu cha kusambaa kwa taarifa na matukio ya vurugu.

Your Comment